Ni wiki ambayo Bunge litaamua juu ya hatua za
kuchukua dhidi ya vigogo wa Serikali ambao wamekuwa wakitajwa kuhusika
na ufisadi huo wa kuchota au kunufaika na Sh306 bilioni katika Akaunti
ya Tegeta Escrow iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ripoti hiyo inayosubiriwa, itawasilishwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), inayoongozwa na Zitto Kabwe, ambayo itatoa mapendekezo juu ya hatua za kuchukua.
Wabunge wa vyama mbalimbali, jana walikuwa na vikao kadhaa wakijipanga jinsi ya kushughulikia sakata hilo mara tu ripoti itakapowasilishwa.
Wabunge wa CCM jana jioni walikutana kuwekeana
msimamo kuhusu sakata hilo huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi yao,
hasa walioonyesha kushabikia ripoti hiyo, wamekaripiwa na kupewa
mwongozo wa kuilinda Serikali.
Habari
za ndani zinasema kuna juhudi kubwa zinafanywa ili kuhakikisha Baraza
la Mawaziri halivunjwi kwa mara ya pili, baada ya tukio la mwaka 2007
alipojiuzulu aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kutokana na kashfa ya
Richmond.
Habari zaidi zilisema, juzi kilifanyika kikao
kingine ndani ya Makao Makuu ya CCM, Dodoma kikiwahusisha baadhi ya
wabunge, mawaziri na vigogo wanaotuhumiwa katika kashfa hiyo.
Habari zinasema kikao hicho kilipata muhtasari
kutoka ndani ya PAC lakini hakikufikia mwafaka kutokana na baadhi ya
wajumbe kupinga kujadili suala hilo mbele ya watuhumiwa na bila kupewa
ripoti kamili ya Mdhibiti na Mkaguzi na Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG).
Vilevile, wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) nao walikutana jana kujipanga kwa ajili ya kushughulikia sakata hilo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema wameitisha kikao hicho kuwekeana msimamo.
“Tunakwenda kukutana kama Ukawa ili tuwekeane
msimamo jinsi gani ya kulishughulikia sakata la ufisadi wa Escrow,”
alisema Mnyika.
Ripoti hiyo itawasilishwa huku kukiwa na madai
kutoka Ukawa kuwa imevuja na kusambazwa mitaani na baadhi ya kurasa
zenye majina ya wahusika zikichomolewa ili kuuhadaa umma.
0 comments:
Post a Comment