Tanzania Anthem

Tuesday, 17 June 2014

TAARIFA YA HABARI JUNI 17 YA DODOMA FM ISOME HAPA




DODOMA.
Uchache wa Shule za Msingi katika Kijiji cha  Mpunguzi Mkoani Dodoma umepelekea watoto wengi kujiingiza katika Ajira.

Haya yamethibitishwa na Diwani wa kata ya Mpunguzi Bw,.John Matonya alipokuwa akizungumza na kituo hiki kupitia makala ya amua ambapo amesema kuwa uchache wa shule unapelekea idadi kubwa ya watoto kutoweza kuandikishwa darasa la kwanza hivyo kuwalazimu kubaki nyumbani na kujiajiri.
Aidha Bwana Matonya amesema Halmashauri ina mpango wa kuongeza idadi ya  shule katika Kata hiyo hususani katika Kitongoji cha Mlangwa  eneo ambalo lina idadi kubwa ya watoto ambao hawasomi.
Kwa upande wa wakazi wa Kijiji hicho wanasema kuwa watoto wengi wanajiingiza katika ajira kutokana na kutopatiwa mahitaji muhimu na wazazi  au walezi wao.
Hata hivyo watoto wanaojishughulisha na biashara katika Kijiji hicho wamesema kuwa hali ngumu ya maisha ya nyumbani inayopelekea  kutokupatiwa Elimu ndiyo inayosababisha wao kujiingiza katika ajira wakiwa na umri mdogo.
Na Pasko Mwinje                                                                                              Chanzo DodomaFM
Wamiliki wa vyombo vya usafiri Manispaa ya Dodoma wametakiwa kuhakisha wanatoa tiketi kwa abiria wanaotumia vyombo hivyo.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi kavu SUMATRA kanda ya Kati Dodoma Bw. Bahati Musiba alipokuwa akizungumza na kituo hiki ambapo amemtaka  kila mmiliki wa chombo cha usafiri ahakikishe anatoa tiketi kwa abiria.
Aidha Bw.Musiba  amesema watakao kiuka utaratibu wa  kutotoa tiketi kwa abiria mamlaka hiyo itawachukulia hatua kali za kisheria.
Kwa upande wa Abiria pamoja na Wamiliki wa vyombo vya usafiri  wamesema suala la tiketi ni muhimu kwani linatoa  utambulisho baina ya abiria na chombo husika.
Na Nazael Mkude                                                                                       Chanzo DodomFM

Serikali imetakiwa kupunguza matumizi yake ya kawaida kwenye bajeti ya mwaka wa fedha  2014/15 ili fedha hizo zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Kigoma Mjini Bwana Peter Serukamba alipokuwa akichangia  hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15 iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Wizara ya fedha na uchumi.
Aidha Bwana Serukamba ameitka serikali kuchukua maamuzi magumu kuhusiana na suala zima la reli ya kati ili lipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu Bi Leticia Nyerere akichangia hotuba ya bajeti amesema iwapo rasilimali zilizopo  nchini zikitumiwa vizuri  itasaidia kupiga hatua kubwa ya  maendeleo na kuinua uchumi wa nchi.
Na Lucas Godwin                                                                                                             Chanzo Bunge

KITAIFA
Mahakama imefanya mabadiliko katika kanuni za uendeshaji wa mashauri ya watoto, kwa kuandaa kanuni mpya ili  kuharakisha usikilizwaji na uamuzi wa kesi zinazowahusu.
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman amesema hayo wakati wa ufunguzi wa warsha ya uendeshaji wa mashauri yenye masilahi kwa umma kwa majaji wa Mahakama Kuu, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema hatua hiyo imetokana na utafiti uliofanyika katika nchi tatu za Afrika Mashariki kuhusu uendeshaji wa mashauri yenye masilahi kwa umma ambao umeonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa.

Jaji Othman amesema mbali na kesi hizo zenye masilahi kwa umma, kesi nyingine ambazo Mahakama inazipa kipaumbele katika kuhakikisha kuwa zinashughulikiwa haraka ni kesi za jinsia na watoto.
Na Zania Miraji 
                                                                                                    Chanzo Mwananchi
KIMATAIFA
Shambulizi lingine limetokea katika eneo la Mpeketoni karibu na Lamu  pwani ya Kenya na kusababisha vifo vya watu 10.
Jeshi la Polisi limesema washambuliaji wa kundi la Al Shabaab wamekiri kufanya shambaulizi hilo  ambapo walivamia kijiji kimoja usiku wa kuamkia leo.
Kundi la Al Shabaab limekiri kuhusika na shambulizi hilo ambapo wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa operesheni yao ya mashambulizi itaendelea nchini Kenya.
Shambulizi hili limetokea siku moja baada ya Al Shabaab kukiri kufanya mashambulizi yaliyowaua watu 50 Jumatatu.
Na Zania Miraji                                                                                                     Chanzo BBC
Kiongozi wa mashitaka ya umma wa Misri ameamuru kuachiliwa kwa mwanahabari wa Al-jazeera Abdullah Elshamy kwa misingi ya kiafya.
Bwana Elshamy ambaye anaripotiwa kudhoofika kiafya alikuwa miongoni mwa watu 13 ambao mwendesha mashtaka mkuu aliamua kuwaachilia kwa misingi ya kiafya siku ya Jumatatu ambapo 12 waliosalia ni waliokuwa wakiunga mkono kundi la Muslim Brother hood.
Bwana Elshamy amekuwa akigoma kula kwa takriban miezi mitano kulalamikia kukamatwa kwake bila kufunguliwa mashitaka.
Alikamatwa mnamo mwezi Agosti mwaka uliopita wakati polisi wakitawanya maandamano yaliyokuwa yakifanywa na waandamanaji waliokuwa wakimuunga mkono rais Mohammed Morsi aliyeondolewa mamlakani.
Stanley msigwa                                                                                                                   Chanzo BBC

Marekani imetangaza kuwa inatuma wanajeshi 275 nchini Iraq kusaidia kulinda maafisa na Ubalozi wake mjini Bagdad.

Tangazo hilo limetolewa wakati maafisa wa Marekani na Iran wakifanya mazungumzo kuhusu hali nchini Iraq katika kongamano linalojadili maswala ya nyuklia mjini Viena.

Rais Obama ameandika barua kwa baraza la Congress kueleza mipango ya kutuma wanajeshi hao 275 mjini Baghdad ambapo amesema jukumu la kikosi hicho ni kulinda raia wa Marekani wanaoishi nchini Iraq na mali zao.
Wanajeshi hao wataendelea kukaa nchini humo hadi hali ya usalama itakapoimarika.
Na Zania Miraji                                                                                                                     Chanzo BBC

Share:

0 comments:

Post a Comment

Blog Archive