DODOMA
Wananchi pamoja na viongozi mbalimbali Mkoani Dodoma wametakiwa kutambua
umuhimu wa kuchangia damu salama ili
kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa
wengine.
Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma Dr.Zainabu Chaula katika maadhimisho ya uchangiaji Damu
yaliyofanyika mwishoni mwa wiki ambapo amesema kuwa kumekuwa na vifo vingi vya
akina mama wajawazito wakati wa kujifungua hivyo ni vyema wananchi wajitokeze kuchangia damu.
Nae Mkuu wa Kitengo cha damu Salama
Mkoani Dodoma Dr.Lea Kitundya amesema siku ya maadhimisho ya uchangiaji wa damu
salama duniani ni siku ya kuwaenzi wale wote wanaojitolea katika suala zima la
kuchangia damu .
Aidha Dr.Lea amewataka wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi katika uchangiaji damu salama kwani
kuna uhaba mkubwa wa ukosefu wa damu .
Kwa upande wa wachangiaji damu
waliohudhuria katika hafla hiyo wamesema
wameipokea vizuri siku ya maadhimisho hayo kwani inasaidia kupunguza tatizo la
watu wanaopoteza maisha yao kutokana na upungufu wa damu na kuwataka watu
wengine wahamasike ili kuweza kuokoa maisha ya watanzania wengine.
Serikali kupitia wizara ya
afya imeanzisha ujenzi wa Hospitali itakayo kuwa na uwezo wa
kutoa huduma zisizo patikana hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu waziri Tamisemi Bw. Agrey Mwanri alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu Elizabeth
Batenga alietaka kujua mwongozo wa wizara ya afya juu ya kulinda afya za wananchi
bila kujali hali zao kichumi .
Aidha Waziri Mwanri amesema kuwa upo mfumo wa rufaa kwa wagonjwa wote
kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali
ya Taifa kwenda kutibiwa Nje ya Nchi kwa
gharama za Serikali.
Pia amesema Serikali ina mfumo wa
kutoa matibabu bure kwa wagonjwa
mbalimbali ikiwemo mama mjamzito na wagonjwa wenye magonjwa sugu kama
saratani,kifua kikuu,kisukari,ukimwi , magonjwa ya akili, pamoja na wazee wa
umri zaidi ya miaka sitini.
Serikali imeeleza kuwa Tanzania
haina budi kuhakikisha inajenga uchumi
wenye misingi imara na uwezo wa
ushindani utakaowezesha kukabiliana na changamoto za maendeleo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa kamati ya bajeti Bwana Andrew
Chenge alipokuwa akitoa taarifa ya kamati ya bajeti bungeni ambapo amesema
Tanzania ni lazima ijenge misingi imara ya uchumi wenye ushindani.
Aidha Bwana Chenge amebainisha kuwa takwimu za mwenendo wa
ukuaji wa uchumi nchini kwa miaka mitatu mfululizo ni wa kuridhisha na umekuwa
kwa wastani wa asilimia 6.8
Kwa upande wake msemaji wa kambi
rasmi bungeni kwa upande wa wizara ya mahusiano na uratibu Bi Ester Matiku amesema ni vyema viongozi kuondoa umaskini
unao wakabili watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao.
KITAIFA
Jeshi la Polisi Zanzibar limesema bomu la kurushwa lililolipuka katika eneo la Darajani na kusababisha kifo
cha mtu mmoja na kujeruhi wengine saba ni la kivita lililotengenezwa kiwandani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini
Magharibi, Mkadam Khamis amesema kwamba uchunguzi wa awali umebaini bomu hilo
hutumika kwa shughuli za kivita na kwamba hiyo ni mara ya pili kwa bomu kama
hilo kutumika katika matukio tofauti Zanzibar.
Hata hivyo, Kamanda Mkadam amesema
hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi
unaendelea ili kuwabaini wahusika na kupitia mikanda ya video na kusikiliza
mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Sheikh Kassim ili kuwasaidia kubaini chanzo.
Bomu hilo lilirushwa na kulipuka
muda mfupi baada ya watu kuhudhuria mawaidha msikitini yaliyokuwa yakitolewa na
Sheikh Kassim Mafuta kutoka Tanga ambaye
kutokana na tukio hilo, amesitisha ziara yake Zanzibar kwa sababu za kiusalama.
KIMATAIFA
Shirika la
uhamiaji la kimataifa limesema linahitaji dola milioni 97.2 za kimarekani ili
liendelee kutoa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini hadi mwezi Desemba.
Shirika
hilo limebadilisha makadirio ya fedha linazohitaji kutokana na hali halisi
nchini Sudan Kusini ambapo zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao
wanahitaji msaada wa kibinadamu.
Kwa
mujibu wa Shirika la uhamiaji la kimataifa zaidi ya watu elfu 94 wanahifadhiwa
katika sehemu zinazowahifadhi watu wanaohitaji ulinzi.
Watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Kiislamu wameshambulia kituo cha
polisi, mahoteli na vijiji mbalimbali mjini Mpeketoni pwani ya Kenya .
Shambulizi
lilifanyika usiku wa june 15 ambapo watu
waliokuwa wamejifunika nyuso zao wakiwa wamejihami vikali walivamia vituo vya polisi ,hoteli na benki.
Duru
kutoka kisiwa cha Lamu zimearifu kuwa wapiganaji hao walifika katika malori
mawili na kurusha kifaa kama bomu ndani ya kituo cha polisi kisha wakavamia na
kuiba silaha.
Baadhi
ya walioshuhudia wamearifu kuwa wameona
maiti kadhaa na majeruhi wengi japo Polisi hawajathibitisha ni watu wangapi
wameuawa.
Shirika
la msalaba mwekundu linasema kuwa hadi kufikia sasa watu 48 wanahofiwa kuuawa
katika shambulizi hilo lililotokea June
15 mwaka huu.
Mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa ya
kuleta utulivu nchini Mali Bw Albert Koenders amesema mchakato wa mapatano nchini Mali unapaswa
kuhusisha watu wote ili kufikia amani ya kudumu.
Bw Koenders
amefafanua kuwa mgogoro wa Mali unapaswa kujadiliwa na mazungumzo ya amani
yaliyoongozwa na Algeria hivi karibuni kati ya serikali ya Mali na waasi na
kusema ni muhimu na ni ya kipaumbele katika kusukuma mbele majadiliano
jumuishi.
Maofisa wa Umoja
wa Mataifa wameipongeza Algeria kwa kazi yake ya kiujenzi katika kuanzisha
amani na maelewano nchini Mali, na kusema ukanda wa Sahel upo hatarini kama
hakutakuwa na amani na usalama nchini Mali.
0 comments:
Post a Comment